Mzee mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja amenusurika kufa baada ya kupokea kipigo
kutoka kwa wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za utapeli.
Tukio hilo limetokea leo majira ya saa nne asubuhi maeneo ya Tazara, Nyerere Road mkabala na Ofisi kuu za Tazara Station, ambapo mzee huyo wa makamo aliwasimamisha madada wanne ambao walikuwa ni wapita njia katika maeneo hayo na kuanza kuzungumza nao kwa lengo la kuwatapeli.
Huku madada hao wakiwa hawajui hili wa lile juu ya mzee huyo, walionekana kumsikiliza na kukubali kile walichokuwa wakiambiwa na mzee huyo.
"Sisi tulikuwa tunapita zetu ndipo pale kwa Bakheressa tulikutana na huyu mzee na yeye akiwa anaelekea huku tunapoelekea sisi, akatusalimia akasema naona ndio mnatoka kazini..? Tukamwambia hatuna kazi..hapa kwenyewe tunatafuta kazi" Alisema dada mmoja alipokuwa anahojiwa na mwandishi wetu
"Basi ndo akatuambia kazi zipo nipeni elfu ishirini( Tsh.20,000/=) nikufanyieni mpango wa nafasi za kazi hapa ninapofanyia mimi"-Aliongeza dada huyo huku akionyesha jengo moja karibu na maeneo yale, ambapo hata huyo mzee alikuwa hafanyi kazi pale.

Mzee tapeli mwenye shati jeupe na kofia, pembeni ni mmoja wa madada hao ambao walitaka kutapeliwa na mzee huyo
"Akatutolea makaratasi akaanza kutuuonyesha kwamba ametoka kumuunganisha mtu sasa hivi pale kazini. Hivyo na sie tumpatie hiyo hela ili akatufanyie mpango. Akasema atamchukua mmoja kati yetu ataondoka nae kwenda kufanya hiyo mipango halafu sisi tuendelee kumsubiri hapa hapa"- Aliongea dada mwengine kwa uoga bila kutaja jina lake
"Akatutolea makaratasi akaanza kutuuonyesha kwamba ametoka kumuunganisha mtu sasa hivi pale kazini. Hivyo na sie tumpatie hiyo hela ili akatufanyie mpango. Akasema atamchukua mmoja kati yetu ataondoka nae kwenda kufanya hiyo mipango halafu sisi tuendelee kumsubiri hapa hapa"- Aliongea dada mwengine kwa uoga bila kutaja jina lake

Wakati tapeli huyo akiendelea kutumia mitego yake kuwaingiza mjini ama kuwapiga changa madada hao, ndipo walipotokea watu wawili ambao walikuwa wanamfahamu vizuri mzee huyo juu ya tabia yake hiyo. Katika hali ya kuwaonea huruma wale madada, ikabidi watu hao wamfuate mzee huyo na kuingilia kati maongezi aliyokuwa akiwaongelesha madada wale.
Baada ya kuona mambo yashabadilika, tapeli yule akatafuta upenyo wa kukimbia..lakini alikuwa ameshachelewa, kwani watu wale waliweza kumdhibiti kisawa sawa na kuanza kumshutumu juu ya utapeli ambao alikuwa akitaka kuwafanyia madada wale. Punde watu wakajaa eneo lile na kuanza kutaka majibu sahihi toka kwa mzee yule. katika hali ya kujaribu kujitetea akasema yeye sio tapeli bali anafanya kazi BP.
"Mimi sio tapeli jamani, nafanya kaazi BP na wala sijataka kuwatapeli hawa madada" Alijitetea mzee huyo kwa wasiwasi mkubwa wa kupoteza maisha yake mbele ya wananchi wale ambao walikuwa washamzunguuka. Lakini kauli yake ya kusema anafanya kazi BP ilimtia tena hatiani mzee huyo baada ya watu waliomzunguuka kutaka aonyeshe kitambulisho chake kama uthibitisho wa yeye kufanya kazi BP kama alivyojielezea. Aliposhindwa kufanya hivyo, ndipo wananchi hao walianza kumuangushia kipigo cha paka mwizi.
Tapeli huyo akipokea kipigo toka kwa wananchi wenye hasira kali.
"Huyu mzee tunamjua na hii ndio tabia yake, ameshawatapeli wanawake kibao hapa. Anatoka nao huko anakuja kusimama nao hapa akitumia ofisi zilizopo eneo hili kujifanya kwamba anafanya kazi humo na kuwachukulia pesa zao kwa uongo wa kuwaunganishia kazi na kuwatelekeza" Alisema mmoja wa wananchi hao aliyejulikana kwa jina la Masamaki bodaboda( mwenye miwani juu pichani )
"Kazidi huyu jamaa mimi namjua mpaka Kariakoo ndio shughuli zake hizo hizo za utapeli. Ebu ona madada wa watu kukosa sisi walikuwa tayari washatapeliwa hawa!..Anatuharibia maskani yetu tunaonekana sisi tunaokaa hapa ndio tunawatapeli hawa madada..sasa leo ngoja tumpe kipigo ili akome!" Alisema kwa jazba mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la White
Baada ya kupokea kipigo, tapeli huyo mzee alipata upenyo wa kunyanyuka na kukimbia akikatiza barabara mbili bila kuangalia magari yatokayo kushoto wala kulia. Bado kidogo agongwe na gari baada ya kuanguka katikati ya barabara. Alinyanyuka na kutimuwa mbio kupitia geti kuu la Tazara na kutokomea pasipojulikana. Inasemekana mzee huyo anaishi maeneo ya Tandika na utapeli ndio shughuli yake kubwa anayojishughulisha nayo hapa mjini.
TAADHALI: Watu wote mnapaswa kuwa makini pindi unapoongeleshwa na mtu ambaye humfahamu kwa kukutana nae tu barabarani! Hasa wanawake wamekuwa wepesi sana kusimamishwa na kusikiliza kila wanachoambia hata kama mtu hawamjui. Kuweni makini kwani wengi wao ni matapeli na wala hawana uwezo wowote wa kuwasaidia zaidi ya kuwaibia pesa ama simu zenu na kuwakimbia!
No comments:
Post a Comment