ads

Slider[Style1]

Style2

Style3[OneLeft]

Style3[OneRight]

Style4

Style5

                                                       


Simulizi kali ya kutisha iliyoandikwa na Amir Malick, imeanza leo sehemu ya kwanza. Fuatilia na usikubali kupitwa na simulizi hii ya kusisimua hapa hapa kwenye ukurasa huu

STORY: JINI CHEKETU
MTUNZI: AMIR MALICK
MOBILE: 0719-050588


Ghafla kichwa kikaanza kumuuma. Jasho likaanza kumtoka na miguu kuishiwa nguvu kama mtu aliyepigwa na marungu mazito!, alitamani kukaa chini lakini maumivu makali ya kichwa yaliyokuwa yakizidi kila baada ya sekunde yalimfanya atupe chini mfuko wake wa rambo ambao alikuwa amebeba madaftari yake ya shule na kushika kichwa..alitaka kupiga kelele lakini alihisi koo limemkauka na hakuna ukelele wowote ambao angeweza kuutoa! Mwili ukamuisha nguvu na mapigo ya moyo kumuenda kasi..aliogopa sana lakini hakujuwa anachokiogopa. Aligeuka kushoto na kulia kama mtu anayetafuta njia ya kutokea..lakini hakuiona, alihisi kama anaguswa mgongoni..aligeuza mwili mzima mzima na kugeuka nyuma kwa kasi..lakini hakuona mtu. Woga ulizidi kumjaa, mwili ukazidi kumtetemeka. Hakuona msaada wowote zaidi ya pori kubwa lililomzunguuka na kuacha kinjia kidogo chembamba kilichonyooka. Jua la saa saba lilizidi kumchoma na kuhisi kama kichwa kinataka kupasuka, vivuli na mivumo ya miti vilizidi kumchanganya, sauti za ndege waliokuwa wakilia kwenye pori lile zilionekana kuzidi kumtisha. ASHURA hakuwa kabisa kwenye Dunia hii tuliyopo sisi..bali alikuwa kwenye dunia nyengine ya ajabu ambayo hata hakuweza kutambua aliingiaje.  Umri wake mdogo wa miaka kumi lakini aliweza kutambuwa kwamba yupo kwenye hatari kubwa. Hatari ambayo inaisakama maisha yake. Masikini ya Mungu hakuweza kujuwa afanyaje katikati ya pori lile. Akapata wazo moja tu.. “KUKIMBIA”
Akarudia tena kuangalia mazingira yaliyokuwa yamemzunguuka koshoto na kulia, bila ya kukumbuka mfuko wake wenye madaftari ya shule ambao ameubwaga pale chini.. kama mtu aliyechanganyikiwa akatimua mbio kwa kasi ya ajabu kuifuata njia ile nyembamba. Njia ambayo anaipita kila siku tangu siku ya kwanza anaanza darasa la kwanza katika shule ya Msingi  Msanga Mtimle..tena akipita kwa madaha yote! lakini leo ajabu imekuwa tofauti na kujikuta yupo katika hali asiyoielewa

Tangu alipoanza mbio zile hakufikiria kuangalia pembeni wala kugeuka nyuma, badala yake alichokuwa akikihitaji ni kufika nyumbani tu. Hakuweza kukutana na mtu yoyote njiani..hakufikiria kusimama popote pale, kwani aliamini hana njia nyengine ya kujiokoa zaidi ya kukimbia, hata alipojaribu kujiuliza sababu iliyokuwa ikimfanya akimbie hakupata jibu sahihi..lakini nafsi yake ilimuamuru hivyo..na hakuona sababu ya kupinga, alizidi kuongeza kasi huku akiwa ametawaliwa na woga mkubwa.. ilimchukuwa kama dakika kumi akawa amefika nyumbani kwao. Hakutaka hata kusimama pale kwenye uwanja wa nyumbani kwao, badala yake kwa kasi ya kimbunga akampita mama yake mzazi aliyekuwa amekaa kwa pembeni akiosha vyombo.. akapitiliza moja kwa moja mpaka ndani kwenye kijumba chao cha udongo. Na kama laiti ile nyumba ingekuwa ina mlango mwingine wa kutokea uani,,basi angepita na kuendelea kukimbia

“We Ashuraa!!!” aliita mama yake kwa taharuki huku akiwa hana uhakika kama aliyepita pale kwa kasi ile ni Ashura kweli ama lah..!
“Ashuraaaa..!” Aliita tena bila kujibiwa. Alipoona hajibiwi ikabidi anyanyuke, akaangalia kule alipotokea Ashura kama pengine palikuwa na mtu anamkimbiza au kitu chochote kilichomfanya mwanawe akimbie vile, lakini hakuona kitu, akakaguwa tena huku na huko lakini wapi hakukuwa na kitu.

“Tayari hivyo ushachokoza watoto wa watu unakimbilia ndani..!!” Alisema mama Ashura kama kujaribu kuhisi labda jibu lingekuwa sahihi na alivyofikiria kwamba Ashura anakimbia baada ya kuanzisha ugomvi na watoto wenzie huko alipotoka. Ni kawaida kwa watoto kucheza na kugombana hiki na kile na hata kufikia kukimbizana. Huku akijifunga khanga yake vizuri mama Ashura akuvuta hatua za haraka haraka kuelekea ndani

Kama mtu anayeanzwa na uchizi wa ghafla, alijikusanya akajibana kwenye pembe ya ukuta wa udongo mwisho kabisa kwenye chumba kile bila kujali kama anachafua shati lake jeupe la shule alilolivaa, huku vipande vya udongo na vumbi vikiwa vinamdondokea.. akavuta shuka kubwa kuukuu ambalo lilikuwa halieleweki hata rangi yake baada ya kuwa la zamani mno na hata kuchakaa toka pale kwenye kitanda chao kidogo cha kamba, akajikunja kama paka aliyenyeshewa na mvua, akajifunika gubigubi akatulia kimya

“Ashura!” Aliita tena mama yake baada ya kuingia ndani na kumuona mwanawe akiwa amejificha kule pembeni bila ya kuonekana hata unywele mmoja. Taratibu kwa tahadhari yenye uwoga akasogea mpaka pale alipokaa Ashura, akafunua lile shuka kwa kutumia nguvu kidogo. Akamkuta Ashura anatweta huku akitetemeka mwili mzima, hakuonekana kutoka jasho japo alitoka kukimbia mbio ndefu. Akawa ameendelea kujikunja vile vile huku kichwa chake akiwa amekifutika kwenye magoti yake na kujizunguushia mikono yote miwili. Hali ile ilizidi kumchanganya mama yake asijuwe mwanawe amepatwa na nini, hakuna hata siku moja aliyowahi kurudi akiwa katika hali hii, leo imekuwaje tena! Akatoka nje tena akaangalia mazingira kama kuna chochote kinachokuja upande wa nyumba yao..lakini hakuona kitu. Alipohakikisha kwamba kupo sawa akaingia tena ndani kisha akasindika kimlango chao kilichokuwa kimefumwa kwa makuti, na kwenda tena pale alipo mwanawe

“We Ashura..mbona hivyo! Kulikoni?” Ashura hakujibu kitu wala kutikisika badala yake alitulia tuli vile vile
“Ashura mwanangu mi naongea na wewe..ebu niambie kuna nini?!” Alihoji tena mama yake kwa shauku kubwa ya kutaka kujuwa sababu ya mwanawe kuwa katika hali ile. Alipoona hajibiwi akamshika kichwa na kujaribu kumuinua uso wake. Kichwa cha Ashura kilikuwa cha moto kama chungu kilichotoka kuepuliwa jikoni, mama yake akagundua hilo. Akahisi mwanawe yupo kwenye tatizo, akakaa chini

“Ashura mwanangu..mimi ni mama yako ebu niambie una nini?!” Alishusha sauti huku akimsogeza mwanawe na kumkumbatia kujaribu kumtoa hali aliyokuwa nayo ili aweze kumwambia kilichomsibu. “walitaka kukubaka..?” Muda wote huo Ashura alikuwa amenyamaza kimya huku akitetemeka na joto kuzidi kuutawala mwili wake. Alionekana ni mwenye hofu kubwa sana na kuna vitu vilikuwa vinapita kichwani mwake kama mkanda wa sinema..lakini kila akitafakari kupata jibu ya vitu vile hakuweza kuambua kitu, tena kila alipozidi kufikiria aliona kiza kizito kinatanda mbele na kufanya macho yake kupoteza nuru taratibu. Alikuwa anatamani kumwambia mama yake lakini alihisi mdomo usingefunguka..au hata kama ungefunguka basi sauti isingetoka.. na kama sauti ingetoka basi maneno yasingeeleweka. Alijaribu kuanza kupangilia maneno lakini alihisi mdomo umeshonwa nyuzi nyingi nzito zinazofanya ashindwe kuinua midomo!.. mara aliona kama kuna mtu amemsimamia anamkataza asiseme kitu. Akajikakamua akameza funda la mate, akageuza shingo akamuangalia mama yake usoni kwa macho makali yenye mshangao kama vile anataka kuhakikisha kwamba yule aliyopo pale ni mama yake kweli ama lah..,macho yalikuwa yamebadirika rangi na kuwa myekunduuu kama amemwagiwa maji ya pilipili kiswasa! Mishipa ya kichwa ilikuwa imemsimama kisawasawa na pua zikawa zinamcheza kama nguruwe pori anayegombana na shina la muhogo. Alikaza macho na kumuangalia mama yake kwa sekunde kadhaa, alipohakikisha kuwa ni mama yake kweli, tena mama yake mzazi.. huku machozi yakimtoka akajitahidi kujaribu kufungua midomo na kuanza kusimulia kilichomkuta.

JE ASHURA AMEKUTWA NA NINI? ATAWEZA KUSEMA NA KUMWAMBIA MAMA YAKE? FUATILIA TENA SEHEMU YA PILI YA SIMULIZI HII SIKU YA KESHO KUTWA JUMANNE


About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment


Top