ads

Slider[Style1]

Style2

Style3[OneLeft]

Style3[OneRight]

Style4

Style5

                                               


ILIPOISHIA:
Macho yalikuwa yamebadirika rangi na kuwa myekunduuu kama amemwagiwa maji ya pilipili kiswasa! Mishipa ya kichwa ilikuwa imemsimama kisawasawa na pua zikawa zinamcheza kama nguruwe pori anayegombana na shina la muhogo. Alikaza macho na kumuangalia mama yake kwa sekunde kumi, alipohakikisha kuwa ni mama yake kweli, tena mama yake mzazi.. huku machozi yakimtoka akajitahidi kujaribu kufungua midomo na kuanza kusimulia kilichomkuta.

ENDELEA
Swala la shule vijijini lilikuwa ni tatizo kubwa katika miaka hiyo ya tisini. Watoto wengi walionekana kujishughulisha na kazi nyengine za nyumbani, kulima na kulinda mashamba lakini sio kwenda shule. Si kwamba walikuwa hawataki kusoma..hapana, bali shule zenyewe hazikuwepo nyingi vijijini, na hizo chache zilizokuwepo zilikuwa mbali sana kiasi kwamba hakuna mzazi angemruhusu mwanawe afunge safari ya pori kwa pori kwenda na kurudi huko kila siku! Hivyo ikapelekea watoto wengi kuja kuanza shule ya msingi wakiwa na umri mkubwa pindi shule hizo zilipoanza kuingia karibu na vijiji vyao. Mmoja kati ya watoto hao alikumo ASHURA. Ashura binti Sued Gamba, mtoto wa mkulima katika kijiji cha Mtimle Msanga mkoani pwani.

Ashura alianza darasa la kwanza akiwa ni mwenye bidii nyingi mno, hakukatishwa tamaa na umri wa miaka kumi aliokuwa nao, wala hakuchoshwa na hali ya baridi la alfajiri na kulowa umande kwenda shule, mwendo wa kilometa mbili aliokuwa akitembea kila siku alikuwa ameshauzoea. Alisoma kwa bidii na kujituma zaidi kwenye masomo na ndani ya kipindi kifupi tu kila mtu kijijini hapo alipata habari zake juu ya ufanisi wake mzuri darasani, wazazi wake walifurahi na kuamini wamepata mkombozi wa maisha yao baada ya kaka zake wote kutimkia mjini karibu miaka mitano iliyopita huku wakiwa hawana elimu, wala maisha yoyote mazuri zaidi ya kutangatanga na jiji bila ya kuleta chochote kijijini kwa wazazi wao.

“Soma mwanangu..wewe ndo tunakutegemea uje kutuokoa wazazi wako hapo baadae” alisema mama Ashura akimwambia mwanawe huku akipekuwa daftari la hesabu na kuona amekosa hesabu moja tu kati ya hesabu kumi walizofanya siku hiyo
“Kama hujaelewa uwe unamuuliza mwalimu atakuelewesha..sawa? na usiwe mgomvi kwa watoto wa watu wala usijiingize kwenye makundi ya wanaume! Sawa mwanangu?..wanaume wana ‘ukimwi’ watakuambukiza utakufa!!” Mara kwa mara alikuwa akitumia muda mwingi kumsihi mwanawe na hata inapobidi kutumia vitisho vikali ili kumuhepusha kujiingiza katika makundi yasiyofaa na kuharibikiwa

Ilikuwa imeshatimu saa saba kamili mchana ambapo wanafunzi wote wanaruhusiwa kurudi majumbani mwao.
Kama ilivyo kawaida Ashura na baadhi ya marafiki zake wakajikusanya, walipo hakikisha wametimia, wakaanza safari ya kurudi nyumbani. Mwendo wa kama dakika kumi na tano Ashura akajikuta amebaki peke yake baada ya marafiki zake wote kila mmoja kuchapuka njia yake kuelekea kwao. Mara zote alijisikia mnyonge kutengana na rafiki zake hao, alitamani wangekuwa wanarudi wote mpaka nyumbani na kuishi pamoja kila siku, kwani alishawazoea kucheza michezo ya hapa na pale njiani..wakati mwengine alijipa moyo kwamba kesho watakutana tena, akawa kila wanapoachana anaombea asubuhi nyingine ifike ili aweze kwenda shule na kuonana nao. hiyo nayo ikawa ni sababu nyengine kubwa iliyomfanya azidi kuipenda shule. Hivyo hakuwa na jinsi kwani kila mtu alikuwa ameshafika kwao na kubaki yeye peke yake kuendelea na safari kurudi nyumbani. Mkononi akiwa ameshika mfuko wa naironi wenye rangi ya bluu( maarufu kama mfuko wa rambo ) ambao alikuwa amebebea madaftari yake ya shule

Safari aliyokuwa amebaki nayo ilikuwa ndefu kidogo, hivyo hakutaka tena kuendelea na michezo ya njiani ukizingatia alikuwa yuko peke yake, alinyoosha moja kwa moja akiifuata njia nyembamba iliyokatiza katikati ya pori kuelekea nyumbani. Njaa ilikuwa ni sababu nyengine iliyomfanya azidishe mwendo kuwahi chakula. Jua kali la saa saba mchana lilikuwa linawaka na kufanya barabara kukakamaa na kuwa ya moto! Tangu ahaidiwe kuwa ataletewa viatu vya shule na shangazi yake anayeishi Majoye jijini Dar es Salaam ni muda mrefu umepita bila kuletewa hata kandambili moja, hivyo akawa hana jinsi kwenda shule pekupeku, jua likazichoma nyao zake kisawasawa!

“Shikamoo bibi” Alimwamkia bibi mmoja aliyekutana naye njiani huku akisimama na kusogea pembeni kumpisha bibi yule apite kwanza kisha na yeye ndio apite. Hiyo ni moja ya tabia na heshima ambazo karibu watoto wote wa vijijini wanafundishwa kuifuata

“Marahabaa mjukuu wangu..ndio unatoka shule?” Bibi aliitikia salamu ile na kumuuliza huku akiwa amekunyata mikono yake nyuma. Alikuwa ni bibi mzee sana mwenye umri wa miaka inayofikia themanini na zaidi. Uzee aliokuwa nao ulimfanya apinde mgongo na kumfanya kuwa na kimo kifupi huku akitembea kwa hatua fupi na mwendo wa taratibu mno. Ashura hakuwa anamjua bibi huyu, ila alimsalimu kwa heshima kama bibi yake

“Ndio bibi natoka shule narudi nyumbani” Alijibu Ashura. Baada ya hapo kimya kikatanda.
Ni tofauti na alivyokuwa akifikiria Ashura labda yule bibi angeongeza sentesi nyengine au kumuuliza ama kumwambia kitu kingine chochote baada ya kumjibu lile la kwanza..lakini yule bibi hakuuliza tena swali lingine na wala hakuonyesha kama alikuwa anaongea na Ashura, badala yake akampita taratibu na kuendelea na safari yake kimya kimya.  Japo alikuwa ni mtoto mdogo lakini aliweza kushangazwa na hilo ambalo kwake aliliona si la kawaida, baada ya kumpita hatua kama tatu akajikuta anageuka nyuma na kumuangalia vizuri yule bibi, lakini ajabu hata alipogeuka hakumuona! Aliangalia ile njia yote ilikuwa nyeupee lakini yule bibi haonekani! Ashura alishangaa maajabu yale. Akavuta kumbukumbu zake haraka haraka akaamini kwamba alikuwa anaongea na bibi sekunde nne tu zilizopita, na yule bibi alikuwa anaelekea kule ambapo yeye alikuwa anatoka..sasa iweje wapishane sekunde hii hii na sekunde hii hii asimuone tena!? Ukizingatia mwendo aliokuwa akitembee yule bibi ni mwendo wa kujikongoja mno ambao hata sisimizi angemvuka! Kweli uzee aliokuwa nao angeweza kutembea haraka kwa speed ipi mpaka kumaliza njia yote bila kuonekana!? Tena ni njia ambayo imenyooka ya kuweza kumuona mtu hata aliyekuwa umbali wa mita mia mbili! Inakuwaje yule bibi asionekane?!

“Ina maana ameyayuka?!” Aliwaza lakini hakutaka kuamini hilo moja kwa moja. Alijaribu kuangalia tena huku na huko labda pengine atakuwa amechapuka njia nyingine..lakini hakukuwa na njia nyingine zaidi ya hiyo. Alitamani kumuita lakini akasita. Alitulia akabana pumzi kama sekunde tatu akisikilizia kwa umakini mkubwa kama atasikia hata ishara yoyote ya yule bibi akitembea..lakini wapi! Eneo lote lilikuwa kimya na hakukuwa na mtu mwingine yoyote zaidi ya yeye Ashura peke yake. Akahisi mwili unamwisha nguvu na mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi kwa uoga
******************                          *********************                    *********************

“Yule bibi ndio sijamuona tena!.. na mimi hapo hapo kichwa ndio kikaanza kuniuma ndio nikakimbia..” Kwa kukwama kwama Ashura akamaliza kumuadithia mama yake kile kilichomtokea njiani huku machozi yakimtoka. Mama yake akashusha pumzi nzito akajuwa mwanawe amepatwa na tatizo.
“Loh! Pole mwanangu.. lakini sasa hivi unajisikiaje?”
“Kichwa kinazidi kuniuma mamaa..”Alisema Ashura huku akilia “Mwili hauna nguvu na miguu mizitoo..halafu naona kizunguzungu”

Mh! Mama yeke akastuka, akafikiria haraka haraka akaona anatakiwa atoe msaada kwa mtoto wake haraka sana la sivyo mambo yanaweza kubadilika muda si mrefu. Kwani joto lilizidi kuongezeka na Ashura kuzidi kuregea. Akafikiria dawa ya kumpa lakini akakumbuka ndani hakukuwa hata na nusu ya kidonge cha panado. Akapata jibu ni lazima ampeleke kwa mtaalamu wa jadi haraka sana! Akatoka nje kuangalia kama anaweza kupata msaada hata wa mpita njia mwenye baiskeli ili aweze kumsaidia kumbeba..lakini hakuna mtu aliyekuwa anapita barabarani! Akawa kama amechanganyikiwa, hajui nini afanye kumuokoa mwanae, kila nyumba ya jirani aliyofikiria kwenda ilikuwa mbali na akili haikumruhusu kwenda mbali huku akimuacha mwanawe peke yake katika hali ile. Kengere ikagonga kichwani mwake kwamba mwanawe yupo kwenye hali tete!

“Huyu baba yako naye tabia zake hizi sijui ataziacha lini?!” Alisema peke yake kwa hasira mama Ashura huku akijaribu kuchungulia huku na kule kama atapata hata msaada wa mpita njia pale nje

“Ye kila akienda shambani muda wa kurudi hafiki nyumbani kwake kwanza mpaka apitie vijiweni..matokeo yake ndio kama hivi mi nipo peke yangu hapa sasa nafanyaje eeng’?!” Alizidi kuhamaki na kupagawa huku akimtupia lawama mume wake ambaye mpaka muda huo alikuwa bado hajarudi kutoka shamba

“MAMAA.. MAMAAAAAAAAAAAAA….!!!” Kelele zilisikika kutoka ndani alipokuwa Ashura. Mama yake akakurupuka mbio kurudi ndani kujuwa nini kilichomfanya mwanawe kupiga kelele zile

“Vipi?..kuna nini!?..Ashura! Ashuraa!! We Ashura!!!” Aliuliza kwa mshangao na kuita huku akiwa amemshika mabegani na kumtingisha. Lakini masikini Ashura wala hakuonekana kutingishika wala kupepesa macho, badala yake akawa ameganda amebutua macho tu kama mtu aliyekuwa akiona maajabu ya mwisho ya Dunia.
“Ashuraaa!!!” Aliita tena bila mafanikio

ITAENDELEA IJUMAA SAA 12 JIONI
JE ASHURA AMEPATWA NA NINI? MZIMA AU AMEKUFA? MAMA YAKE ATAFANYAJE?
USIKOSE SEHEMU YA TATU YA SIMULIZI HII YA KUSISIMUA


About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment


Top