ads

Slider[Style1]

Style2

Style3[OneLeft]

Style3[OneRight]

Style4

Style5

                                                            


ILIPOISHIA:
“MAMAA.. MAMAAAAAAAAAAAAA….!!!” Kelele zilisikika kutoka ndani alipokuwa Ashura. Mama yake akakurupuka mbio kurudi ndani kujuwa nini kilichomfanya mwanawe kupiga kelele zile

“Vipi?..kuna nini!?..Ashura! Ashuraa!! We Ashura!!!” Aliuliza kwa mshangao na kuita huku akiwa amemshika mabegani na kumtingisha. Lakini masikini Ashura wala hakuonekana kutingishika wala kupepesa macho, badala yake akawa ameganda amebutua macho tu kama mtu aliyekuwa akiona maajabu ya mwisho ya Dunia.
“Ashuraaa!!!” Aliita tena bila mafanikio

ENDELEA:
“Ashura vipi kwani mwanangu..?!”
“Mamaa..” Aliita Ashura kwa sauti ya chini “Naomba maji ya kunywa”
Haraka haraka mama yake akaukimbilia mtungi ulipo akachota maji kwa kutumia kata moja ndogo ( Kata ni kifaa kinachotumika kama kikombe kwaajili ya kuchotea maji, hutengenezwa kwa kifuu cha nazi kilichokauka na kukwanguliwa na kusafishwa vizuri kisha kuchomekwa mti mwembamba katikati ndio huwa mshikio wake, mti huu mara nyingi huwa ni mpingo au miti migumu ambayo haina madhala inapoloana na maji )

Kabla hata hajafika mikononi mwake akaivamia kata ile na kuanza kuyafakamia maji kwa fujo kama mtu aliyetoka kufukuliwa kwenye tanuli la moto na sasa alikuwa na kiu ya ajabu
“Niongeze..”
Upesi tena mama yake akaugeukia mtungi na kudidibua tena maji ya kutosha akampelekea. Kama alivyoyapokea mara ya kwanza ndivyo alivyoyapokea tena mara ya pili akayafakamia tena bila kujali mengine yaliyokuwa yakimmwagikia kifuani na kulowesha nguo zake za shule. Mama yake akashangaa sana hali ile, laiti ingekuwa mwanawe yupo kwenye hali ya kawaida basi labda angemuuliza ni chakula gani alichokula mpaka anakunywa maji mengi kiasi kile! Lakini akakumbuka kwamba mwanawe yupo kwenye tatizo na pengine tatizo hilo ndilo linalomfanya anywe maji kiasi kile. Hakutaka kupoteza muda

“unaweza kutembea?”
“Hapana mama nasikia kizunguzungu..”
“Kaa twende!!” Alisema huku akiwa tayari kashageuza mgongo na kuchuchumaa ili mwanawe apande mgongoni

“Vipi tena mbona hivyo?!”
“Mtoto anaumwa..” Alijibu mama Ashura kisha akanyamaza kama mtu aliyekuwa akisubiria swali lingine
“Anaumwa nini?”
“Amekuja anakimbia kutoka shule, anadai kichwa kinamuuma sana, mwili hauna nguvu na anasikia kizunguzungu!”
“Sasa huku mnaenda wapi”?
“Nampeleka kule bondeni kwa Ostaadh Jengo, tena afadhali hata tumekutana..”
“Aaaaggh..! Sasa mke wangu, mtoto anaumwa unampeleka kwa waganga wa kienyeji badala ya kumpeleka hospitali?!”

Alikuwa ni mzee mweusi mwenye urefu na wembamba wa wastani, anaitwa SUED SHAABAN GAMBA. Lakini pale kijijini alikuwa akifahamika zaidi kwa jina la Mzee GAMBA. Huyu ndio baba yake mzazi Ashura na ndiye mume halali wa Bi Amina Mwinyi au Mama Ashura. Mzee Gamba yeye hutoka nyumbani asubuhi na mapema sana mara tu amalizapo swala ya alfajiri, kisha kwenda moja kwa moja mashambani. Mara nyingi akitoka kukagua mashamba na mitego yake hufikia kijiweni kwanza kunywa kahawa na kupiga gumzo na wazee wenzie kisha kupitia msikitini kusali sala ya alasiri halafu ndio hurejea nyumbani mida ya mchana. Wakati huo ndio Mama Ashura naye alikuwa amembeba mwanawe mgongoni wakiwa njiani kuelekea kwa mtaalamu wa jadi, ndipo alipokutana na mumewe akiwa anarudi nyumbani

“Lakini mume wangu huu ugonjwa unavyoonekana sio wa hospitali” Alisema mama Ashura kumwambia mumewe

“ Kwanini usiwe wa hospitali wakati umesema anaumwa na kichwa?! Alihoji Mzee Gamba

“ Amedai wakati anarudi kutoka shule amekutana na bibi mmoja…..

“Aaaaaggh..mke wangu ushaanza na imani zako!..umeshaanza tayari hivyo!!”

Mzee Gamba akamkatisha mkewe kabla hata hajamaliza kusimulia na kuonyesha asivyokubaliana na imani hizo. Siku zote alikuwa hataki kusikia maswala ya mganga wa kienyeji, yeye alikuwa ni muumini mzuri wa dini ya kiislamu mwenye kusali sala tano kila siku iendayo kwa mungu, hivyo hakutaka kabisa imani yake ilale kwa waganga wa kienyeji, kitu kilichokuwa kinafanya wapishane sana na mkewe kila linapoibuka swala kama hilo

“Mzee Gamba lakini ujue wewe hukuwepo nyumbani wakati mtoto anarudi, isitoshe amenisimulia kile kilichomfanya awe katika hali hii..! na mimi kwa jinsi nilivyoongea naye na kumuona hali yake si ya kumpeleka hospitali” Alisema mama Ashura kwa uhakika kujaribu kumshawishi mumewe akubaliane na wazo lake

“Sawa mimi sijakataa maamuzi yako mke wangu, lakini kwanza tumpeleke hospitali, kama huduma ya huko itashindikana basi ndio tumpeleke kwa hao unaowaiita wataalamu wako!”

“Mume wangu, kumbuka hospitali ipo mbali sana! Ni mwendo wa karibu saa nzima kwa miguu, na hapa hatuna usafiri wowote! Unafikiri tutafika saa ngapi? Na kama unavyoona hali ya mtoto hawezi hata kutembea!, unataka tumkose?..enhe? unataka tumkose?!” Hakika uchungu wa mwana aujuae mzazi! Hasa mama ambaye ndiye amebeba ujauzito kwa miezi tisa. Mama Ashura akaonyesha hisia zake juu ya mwanawe kipenzi, akakaza sauti, akaunganisha maneno bila ya kumpa nafasi mumewe. “Acha twende hapo kwa Ostaadh karibu kwanza ampe hata dawa ya kumpoza, kama itakuwa tofauti ndio tufanye mpango wa kutafuta usafiri tumpeleke hospitali”

Maneno ya mkewe yalimchoma moja kwa moja Mzee Gamba. Akamuangalia mwanawe aliyekuwa ananing’inia mgongoni kama kinda la ndege anayehisi baridi kali. Akainua mkono akamgusa kwenye paji la uso, joto kali alilolisikia toka kwenye kichwa cha mwanawe lilimshangaza hata yeye. Akaamini kweli mtoto wao yupo kwenye hali tete

“Ashura mama..!” Aliita kwa unyonge Mzee Gamba. Lakini Ashura hakuitikia, si kwamba alikuwa hataki kuitikia ama anamjeuria baba yake..hapana! bali hali aliyokuwa akiisikia aliona hana nguvu hata ya kuongea. Mzee Gamba akagundua hilo, hivyo hakurudia kumwita tena
*****************                      *****************                    ******************                    *************

“Hodiiiiiiiii we mzaramoo!!..unalala tu jua kali lote hili?!” Alisikika Mzee Gamba akiita huku akichombeza kwa utani baada ya kufika kwenye uwanja wa nyumba ya Ostaadh Jengo

Ostaadh Jengo alikuwa ni mtaalamu mwenye kuchanganya tiba za miti shamba na kitabu cha Quraan. Watu wengi walimsifu kwa dawa zake ambazo zilionekana kuwa ni msaada mkubwa kwa watu wa maeneo yale pamoja na jirani. Hakuwa mzee, yeye alikuwa ni kijana wa makamo na alikuwa akiishi peke yake na shughuli zake kubwa zilikuwa ni uganga

“Ahaaaaaaa Shekhe Gambaa huyooo!..Karibu sana bwana, nilale saizi nina raha gani rafiki yangu?!” Alikaribisha kwa uchangamfu mkubwa huku naye akichombeza utani ule. Kama ilivyo kawaida kwa watu wa pwani kupenda sana matani na kutupiana maneno ya hapa na pale pindi wanapokutana.

“Haya kulikoni tena mbona mmebebana mchana mchana?!” Alihoji Ostaadh Jengo baada ya kutoka nje na kumuona mama Ashura akiwa amembeba Ashura ambaye alikuwa amejikunja mgongoni kama sungura

“Ebu piteni ndani kwanza” Alisema Ostaadh Jengo kabla hata hajajibiwa swali lake huku akiwa kashageuka na kutangulia ndani, kwani moja kwa moja alijuwa ujio ule ulikuwa ni wa kiugonjwa. Bila kuongeza neno lolote Mzee Gamba na mkewe wakamfuata kuingia ndani
***************                    ********************                            *****************

Mama Ashura alitumia kama dakika tatu kuelezea ile hali aliyorudi nayo mwanawe ghafla na pia akamsimulia kuhusu kukutana na yule bibi wakati alipokuwa akirudi nyumbani. Bila ya kupoteza muda Ostaadh akachukuwa kikombe kidogo cha udongo akaenda jikoni akaweka makaa mawili matatu ya moto, akafungua kimfuko chake cha karatasi kilichokuwa kimechomekwa ukutani kwenye fito, akatoa kitu kama chengachenga hivi..akaweka kwenye kile kikombe chenye moto, moshi ukaanza kutoka na harufu ya ubani ikaanza kutawala chumba kile. Kisha akachukua kitabu chake akafunua kurasa aliyokuwa anaijuwa yeye akaanza kusoma polepole kwa umakini mkubwa. Muda wote huo Mzee Gamba na mkewe pamoja na mtoto wao wakawa wametulia tuli wakiangalia

“Anaitwa Ashura vilee enhee..?” Ostaadh aliuliza bila kuinua kichwa kutaka uhakika wa jina. Baada ya kuitikiwa kwamba ni sahihi akaendelea kusoma kile kitabu kwa lugha ya kiarabu. Baada ya dakika kadhaa akainua uso akamwambia Ashura ampe mkono wa kulia. Ashura akafanya hivyo, hapo Ostaadhi hakuendelea kuangalia kile kitabu, badala yake akamkazia macho Ashura huku amemshika mkono na kuendelea kuongea maneno kwa lugha ile ile. Baada ya hapo akamuachia mkono na kumshika kichwa huku akiendelea kuongea maneno ya kiarabu aliyokuwa akiyajuwa yeye mwenyewe. Ghafla machozi yakaanza kumtiririka Ashura kama mtu aliyefungua koki ya bomba la maji, hakua akilia kwa sauti..bali ni machozi tu yaliyokuwa yakimwagika yenyewe. Baaada ya dakika kama tano Ostaadh akaondoa mkono kichwani mwa Ashura na kunyamaza kama sekunde tatu kisha akashusha pumzi nzito kama tairi la gari linalopata pancha ghafla! Akajiweka vizuri kisha akasema

“Mtoto wenu ana tatizo kubwa..” Alinyamaza kidogo kisha akaendelea “Na kusema ukweli mimi binafsi sina uwezo wa kulimudu tatizo hili!..kwanza najisikia kuogopa kwa hili nililoliona hapa”
“Ostaadh sijakuelewa..una maana gani?!” Alihoji kwa mshangao Mama Ashura kama mtu asiyetaka kukubaliana na kile anachokisikia. ( Kutoka Msanga kwenda Kimanzichana ni mwendo wa saa moja na nusu kwa pikipiki, kwa miguu inaweza kuchukua mpaka masaa sita.)

“Bwana Jengo ebu tuweke wazi..nini tatizo?!” Aliongeza Mzee Gamba
“kama nilivyosema mwanzo kwamba, tatizo la mwanenu ni kubwa na mimi uwezo wangu wa kulimaliza tatizo hilo ni mdogo mno..” Alijibu Ostaadh Jengo na kuendelea “Nitakachowasaidia nitampa dawa ya kutuliza tu kwa leo..baada ya hapo naona mngefunga safari ya kwenda kimanzichana, kule kuna wataalamu wakubwa zaidi yangu ambao labda wanaweza kuwasaidia zaidi!” Alimaliza kuongea huku akinyanyuka akiwaacha wazazi wa Ashura midomo wazi kwa kutofahamu nini kinaendelea, akafunua kinu kilichokuwa pembeni akatoa majani, akamkabidhi mama Ashura

“Hii dawa mkifika nyumbani mchanganyie na maji ya moto kisha muogeshe na nguo zake hizi hizi..sawa?, halafu maji mengine utamuwekea kwenye kiganja chake atakunywa mara tatu. Dua nililomfanyia hapa pamoja na hii dawa vitamsaidia kumtoa joto na atatulia kabisa, lakini kesho mfanye mpango mumpeleke Kimanzichana kule kuna wakubwa zangu watamsaidia kumaliza tatizo!” Alisema Ostaadh Jengo kwa kumaanisha kile alichokuwa akikiongea

ITAENDELEA>>

NI TATIZO LIPI KUBWA LILILOMKUMBA MTOTO ASHURA MPAKA OSTAADH KUFIKIA KUOGOPA NA KUSHINDWA KUMTIBU? WATAWEZA KWENDA KIMANZICHANA? ITAKUWAJE..? Usikose sehemu ya tatu ya muendelezo wa Simulizi hii ya kusisimua keshokutwa Jumapili saa 12 jioni

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment


Top