Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Muwakilishi wa Kampuni ya Ujenzi wa Bandari ya China yenye Tawi la Ofisi yake Nchini Tanzania Bwana Xu Xinpei.
Muwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi wa Bandari ya China Bwana Xu Xinpei akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif. Bwana Xu Xinpei ameelezea azma ya Kampuni yake kutaka kuwekeza katika sekta na Bandari na Hoteli ya Kimataifa ya Kitalii hapa Zanzibar.
Balozi wa Malawi Nchini Tanzania Balozi Flossie Gomile Tijaonga akisalimiana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kampuni
ya Ujenzi wa Bandari ya Jamuhuri ya Watu wa China { CHEC } imeonyesha
shauku ya kutaka kujenga Bandari kubwa hapa Zanzibar kwa lengo la
kuifanya Zanzibar kuwa katika ramani ya Dunia kwa utoaji wa huduma za
Kimataifa za usafiri wa Baharini.
Kauli
hiyo imetolewa na Muwakilishi wa Kampuni hiyo yenye Tawi la Ofisi yake
Nchini Tanzania Bwana Xu Xinpei wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Bwana
Xu Xinpei alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na eneo zuri la uwekezaji
katika masuala ya usafiri wa Bandari Sambamba na Utalii jambo ambalo
Kampuni hiyo imevutiwa kutaka kuwekeza katika Sekta hizo.
Alisema
mradi huo ambao kitaalamu umekisiwa kugharimu zaidi ya Dola za
Kimarekani Milion 40 unaweza kutoa fursa kwa meli kubwa za Makontena
pamoja na Watalii kutoka Bara la Asia kuitumia Bandari hiyo.
Alisema
hatua hiyo mbali ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya
Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla lakini pia
utaongeza kasi ya Kibiashara katika mwambao wa Afrika Mashariki.
“
Tumekuwa tukishuhudia ongezeko kubwa la uwekezaji ndani ya Visiwa vya
Zanzibar ambalo linaonekana kutawaliza zaidi na wawekezaji wa Bara la
Ulaya wakati uwezo kama huo unawezekana pia kufanywa na wawekezaji wa
Bara la Asia hasa China “. Alisema Mwakilishi wa Kampuni hiyo ya ujenzi
wa Bandari ya China Bwana Xu Xinpei.
Akizungumzia
suala la uwekezaji katika Sekta ya Utalii Bwana Xu Xinpei aliiomba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuipatia Kampuni yake eneo maalum kwa
ajili ya ujenzi wa Hoteli kubwa ya Kitalii hapa Nchini.
Alisema
ujenzi wa Hoteli hiyo unaweza kuamsha ari kwa wageni na watalii kutoka
Kisiwa cha Hainan Nchini China kutembelea Zanzibar kitendo ambacho
kitaongeza kasi ya ushirikiano wa pande hizo mbili.
Alieleza
kwamba Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa ikivunja rekodi ya idadi
kubwa ya watalii wanaotembea na kuzunguuka maeneo mbali mbali ya
Kihistoria Ulimwenguni.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliuomba Uongozi wa Kampuni hiyo kufanya mawasiliano na Mamlaka ya
Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA } na ile ya Ardhi ili kuona
malengo waliyoyapanga yanafanikiwa na kuleta ustawi wa pande zote
mbili.
Balozi
Seif alisema Zanzibar na China na hasa Kisiwa cha Hainan zimekuwa na
uhusiano wa kipindi kirefu kutokana na watu wake pamoja na mimea
inayofanana kimazingira.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa
mazungumzo na Balozi wa Malawi Nchini Tanzania Balozi Flossie Gomile
Tijaonga ofisini kwake Vuga.
Katika
mazungumzo yao viongozi hao waligusia uhusiano na ushirikiano uliopo wa
muda mrefu kati ya Tanzania na Malawi ambao umeasisiwa na Viongozi wa
mwanzo wa Mataifa hayo.
Alisema
bado upo umuhimu wa kuendelezwa kwa uhusiano huo kutokana na Historia
ya kudai uhuru kutoka kwa wakoloni iliyosimamiwa na Rais wa Kwanza wa
Tanzania Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na mwenzake wa Malawi
Marehema Kamuzu Banda.
Naye
kwa upande wake Balozi wa Malawi Nchini Tanzania Balozi Flossie Gomile
Tijaonga alisema Mataifa hayo mawili yamekuwa yakishirikiana kiuchumi
kwa kipindi kirefu.
Balozi
Flossie Gomile alisema Malawi imekuwa ikiitumia Bandari ya Dar es
salaam kwa miaka mingi kupitishia bidhaa na mizigo yake kitendo ambacho
kinastahiki kiendelezaw kwa faina ya pande hizo mbili.
Mwanadiplomasia
huyo wa Malawi Nchini Tanzania ameipongeza Zanzibar na Watu wake
kutokana na mazingira mazuri pamoja na ukarimu wa watu wake unaotoa
fursa ya watu wa mataifa mbali mbali duniani kupendelea kutembelea
Zanzibar.
Alisema hiyo inatokana na Historia kubwa ya Zanzibar katika Nyanja za Kimataifa hasa katika masuala ya Biashara na Utalii.
No comments: