
Viongozi wa
Nchi za Kiafrika katika Makao Makuu ya AU.
Jumla ya nchi 34 kati ya 54 wanachama hai wa AU ni wanachama Mpango wa
Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Katibu Mtendaji wa APRM, Bibi Rehema Twalib akisisitiza jambo alipokutana na waandishi wa habari hivi karibuni.
Na Saidi Mkabakuli
Tanzania,
kama zilivyo nchi nyingi duniani kwa miaka mingi imekuwa mfuasi wa
dhana ya usawa na haki ili kuwa msingi wa maendeleo ya kijamii na
kiuchumi ili kutimiza matakwa ya demokrasia.
Hali
hii imeifanya Serikali kufanya jitihada nyingi za kuboresha dhana hii
licha ya changamoto nyingi zinazokinzana na juhudi hizi za serikali.
Serikali
ya Tanzania kwa kuendeleza ufuasi wake kwa demokrasia na hasa suala
zima la utawala bora, sio tu ilianzisha wizara maalum kwa ajili ya
kusimamia utawala bora pia ilijiunga na Mpango wa Kujipima kwa kutumia
vigezo vya Utawala Bora (APRM) kwa kuwasilisha rasmi maombi ya kujiunga
na mpango huu tarehe 26 Mei, 2004 na kukubaliwa rasmi tarehe 8 Julai
2004, wakati wa Kikao cha Tano cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika.
APRM
ni mpango wa hiari, uliobuniwa na viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika,
kuziwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, kujitathmini katika
utendaji wa shughuli za serikali na shughuli zao nyingine kwa ujumla.
Aidha
mpango huu unalenga kuzipa nchi wanachama, fursa ya kujifunza kutokana
na uzoefu na mafanikio ya nchi zingine za Kiafrika, na hivyo kuziwezesha
nchi husika kuiga sera na mbinu muafaka zilizoleta mafanikio hayo kwa
manufaa ya nchi zao.
Kwa
ujumla, ombi la kufanyiwa tathmini linapofanywa, linaashiria nchi
husika kukubali kufuata misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa
siasa na shughuli za kiuchumi na wakati huohuo, kukubali kufanyiwa
tathmini na Viongozi Wenza wa nchi za Kiafrika.
Hadi sasa nchi 34 kati ya 54 wanachama
wa Umoja wa Afrika zimejiunga na mpango wa APRM. Mpango huo unahusisha
uhakiki katika vipindi mbalimbali (periodic reviews) wa sera, kanuni na
taratibu za utendaji zilizozoeleka (practice) ili kubaini maendeleo
yaliyopatikana katika kutekeleza malengo yaliyokubaliwa katika nyanja za
kisiasa, kiuchumi na utawala wa pamoja wa kibiashara kama
ilivyoainishwa kwenye Tamko la Demokrasia, Siasa, Uchumi na Utawala wa
Pamoja.
Chimbuko
la APRM ni Mpango Mpya wa Maendeleo ya Afrika (New Partnership for
Africa’s Development-NEPAD), ambao unalenga kuliondoa bara la Afrika
kutoka kwenye lindi la umaskini, na kuleta maendeleo. NEPAD imeunganisha
mipango ya maendeleo iliyobuniwa chini ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika,
(OAU), na kuainisha ukosekanaji wa utawala bora kama mojawapo ya
vikwazo dhidi ya maendeleo yanayolikabili bara la Afrika.
Hivyo,
ili kukabiliana na kikwazo hiki, viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika
(UA) walitoa Tamko Kuhusu Demokrasia, Siasa, Uchumi na Uongozi Bora
katika nyanja za uchumi na mashirika ya kibiashara. Tamko hilo pia
linaainisha mkakati wa kufanikisha azma hii, kupitia demokrasia na
utawala bora.
Lengo
la msingi la APRM ni kuhimiza utumiaji wa sera, viwango na miendeno
inayokubalika kitaalamu ili kujenga utengamano wa kisiasa, ukuaji chanya
wa uchumi, maendeleo endelevu na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi wa
kikanda na hatimaye bara zima.
Pia,
APRM inatoa fursa ya kuchangia katika kudumisha utengamano, kuleta
maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kikanda kwa njia
ya kubadilishana uzoefu na kuiga mifano bora ikiwa ni pamoja na kutambua
udhaifu na kutathmini mahitaji ya kuongeza uwezo wa serikali na nchi.
Kwa
kutambua umuhimu wa utawala bora, Mipango na mikakati mingi ya
kimaendeleo na ile ya kupambana na umaskini imekuwa ikijumuisha
kipengele cha utawala bora kama moja ya misingi ya kufikia malengo. Kwa
mfano, moja ya misingi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo (TDV) 2025, kati ya
misingi minne ya utekelezaji, unahimiza uimarishaji wa utawala bora na
uongozi wa haki na kisheria ikiwa ni pamoja na jamii kukataa rushwa,
kuimarisha mifumo ya uongozi na utawala ili kuweza kufikia malengo makuu
ya Dira hiyo.
Pia, kwa upande wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA)
I&II, sifa na misingi yake ni pamoja na Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini wa Mapato; Kuboresha maisha ya watu na Ustawi wa Jamii; na
Utawala bora na uwajibikaji.
Suala
kuu la msingi linalojitokeza katika kila Mkakati ni Utawala bora na
uwajibikaji. Dhana hii ni msingi madhubuti katika kutekeleza mikakati
hii yenye mkondo wa kiuchumi na mingine mingi inayotekelezwa na
Serikali. Hivyo basi, umuhimu wa APRM katika mustakabali wa ustawi wa
jamii ni chanya, kwa kuwa nchi inapata faida ya kujitathmini pale
inapokosea.
Hivi
karibuni Katibu Mtendaji wa Mpango huu (APRM) nchini Tanzania, Bibi
Rehema Twalib alitoa taarifa kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya
vizuri katika utawala bora Barani Afrika.
Akizungumzia
umuhimu wa APRM katika kufikia lengo la msingi la mikakati hii, Bibi
Twalib anasema kuwa ni muhimu kudumisha utengamano, ili kuleta maendeleo
pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kikanda kama njia ya
kubadilishana uzoefu ili kuiga mifano mizuri kutoka nchi zilizopiga
hatua kiuchumi.
Kwa
mujibu wa Bibi Twalib, Tanzania imepata mafanikio katika maeneo ya
Usimamizi wa Uchumi, Maendeleo ya Uchumi-Jamii Demokrasia na Utawala
Bora, Siasa, Uendeshaji wa Kampuni na Masuala Mtambuka kama Afya.
Bibi
Twalib alisema kuwa Tanzania kupitia APRM, imefanya tathmini yake
katika maeneo hayo na kuwasilisha ripoti yake mbele ya wakuu wa nchi
wanachama na kujadiliwa. Akizungumzia mikakati iliyopo katika
kuhakikisha kuwa malengo ya APRM yanakuwa chachu ya kukuza uchumi wa
nchi na kuleta maendeleo kwa jamii ya Kitanzania.
Bibi
Twalib aliongeza kuwa APRM kupitia Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania inaendelea kuendesha tathmini ya utendaji wake na vyombo vyake
kwa uwazi, ukweli na umakini, kulingana na vigezo vilivyowekwa kwenye
Mpango wa Kujipima kwa kutumia Vigezo vya Utawala Bora.
“Kwa kutambua umuhimu katika
kuimarisha utawala bora, Sekretarieti inaendelea kutekeleza Mpango kazi
wa kitaifa wa kujitathmini katika masuala ya utawala bora (African Peer Review Mechanism - National Plan of Action, APRM-NPoA),” aliongeza Bibi Twalib.
Kwa mujibu wa APRM-NpoA, moja
kati ya manufaa ya ya utekelezaji wa Mpango huu ni kubaini mambo mazuri
juu ya utawala bora nchini Tanzania hali inayoongezea imani
(confidence) wawekezaji toka nje ya nchi na wabia wa maendeleo. Hili
moja ya mafanikio ya APRM, maana kwa mujibu wa takwimu kutoka Kituo cha
Uwekezaji Nchini (TIC) mpaka kufikia mwezi Desemba, 2013 kilifanikiwa
kusajili miradi 9,442.
Hatahivyo,
suala la kushirikisha wananchi ni suala lisiloepukika, ambapo, Bibi
Twalib anahimiza suala la nafasi ya wananchi katika Mchakato huu. Bibi
Twalib anasema kuwa, kwa kuwa APRM ina njema ya kupanua wigo wa
demokrasia, na kuwapa wananchi kauli katika maamuzi yanayohusu
mustakabali ya nchi yao.
“APRM
Tanzania inategemea kuwa wananchi watatumia kikamilifu, nafasi
inayotolewa ili kutoa tathmini yao ya kweli, kuhusu yale wanayoyaona
kuwa ni mapungufu ya utendaji serikalini na mapungufu ya utawala bora
nchini kwa ujumla, ili kuiwezesha serikali nayo kuyabaini mapungufu hayo
na kuyachukulia hatua muafaka” anasihi Bibi Twalib.
Anaongeza
kuwa ikiwa wananchi watatumia vyema fursa hizi vizuri, ndipo malengo ya
kuanzishwa kwa Mchakato huu yatakapotekelezwa na kuwezesha kutimia
malengo na misingi ya mikakati ya Serikali ya kuivusha Tanzania kutoka
dimbwi la umaskini.

Wajumbe
wa Bodi na Sekretarieti ya APRM (Tanzania) wakiwa katika picha ya
pamoja na Rais Dkt. Jakaya Kikwete. Kushoto kwa Rais ni Mwenyekiti wa
APRM, Prof. Hassa Mlawa na kulia ni Katibu Mtendaji wa APRM, Bibi Rehema
Twalib.
No comments: