ads

Slider[Style1]

Style2

Style3[OneLeft]

Style3[OneRight]

Style4

Style5


Wanawake wajasiriamali nchini wametakiwa kutengeneza bidhaa ambazo zinahitajika kwa wingi na watumiaji na kuacha kung’ang’ania kutengeneza bidhaa ambazo soko lake ni dogo. Mwito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete wakati wa uzinduzi wa umoja wa vikundi vya kuweka na kukopa Mbagala (UWAMBA) vilivyo chini ya WAMA uliofanyika katika Ukumbi wa Dar Live jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wengi ni upatikanaji wa soko la bidhaa zao lakini kama wataamua kubadilika na kutengeneza bidhaa ambazo zinahitajika kutapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.

“Ni jambo jema kujifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali , lakini kama utaona bidhaa uliyojifunza haina soko unaweza kutengeneza bidhaa nyingine ambayo watu wengi wanaihitaji jambo la muhimu ni kuwa makini katika umaliziaji wa kutengeneza bidhaa nzuri na zinazovutia”, alisema Mama Kikwete.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa vikundi hivyo kwa jamii Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema vikundi hivyo vinatoa mafunzo ya kuweka akiba na kukopa kwa namna ambayo inamsaidia mwanakikundi kujenga tabia ya kujichunga katika matumizi ya pesa na hivyo kuwa na mawazo ya kuweka akiba mara kwa mara.

Aidha Mama Kikwete pia aliwataka wanawake hao kujitokeza kwa wingi kugombea na kushiriki katika chaguzi mbalimbali zinazokuja ili wapate nafasi ya kutoa maamuzi.
Mwenyekiti wa WAMA alisema , “Mkipendana, kushirikiana na kusaidiana mtafika mbali, ondoeni tofauti zenu na kila mmoja asimame na kuweza kumtetea mwenzake, muwe na marafiki wanaopenda maendeleo na kama mwenzako akifanya vizuri usiache kumsifia”.

Akisoma risala ya UWAMBA Halima Abrahman ambaye ni katibu wa kikundi cha Faraja kilichopo Tandika alisema umoja huo wenye vikundi 11 huku wanachama wake wengi wakiwa ni wanawake na wachache ni wanaume ulianzishwa mwaka 2013 wakiwa wanachangia hisa moja kwa shilingi 2000 kwa sasa wana akiba ya zaidi ya shilingi milioni 15.

“Mbali na hisa mapato ya kikundi chetu yanapatikana kutokana na wanachama kufanya biashara mbalimbali zikiwemo za utengenezaji wa sabuni za maji, batiki, mishumaa, vikapu, mifuko ya karatasi, siagi za karanga, kusuka mikeka, unga wa muhogo na achali”, Halima alisema.

Alizitaja changamoto zinazokikabili kikundi hicho kuwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, ukosefu wa ofisi na vifaa vya kuhifadhi taarifa za chama, kushindwa kushiriki katika mafunzo na ukosefu wa masoko ya bidhaa zao.

Ili kukabiliana na changomoto zinavyovikabili vikundi hivyo Mama Kikwete aliwakabidhi vyerehani vinne ambavyo vitatumika kuanzisha mradi wa kushona nguo ambao utawaongezea kipato na Kompyuta moja kwa ajili ya kuweka kumbukumbu zao.

Vikundi vinavyosimamiwa na Taasisi ya WAMA vimetokana mradi wa majaribio wa MWANAMKE MWEZESHE ambao ulianza mwaka 2011 uliolenga kuanzisha mfumo wa vikundi ambavyo vitaweza kutoa fursa za mikopo, mafunzo na kujenga uwezo wa wanachama kujiendesha wenyewe na kuanzisha miradi ambayo itawaongezea kipato.

Mradi huo wa majaribio ulifanikiwa na kuweza kuwafikia watu zaidi ya 1200 kwa kata zilizopo katika maeneo ya Majohe, Gongo la Mboto, Mbagala , Manzese, Temeke na Tandika. Ambapo jumla ya akiba ya zaidi ya milioni 200 zimekusanywa na mikopo ya shilingi milioni 265 imeweza kufikia vikundi mwaka 2013.

Pia mradi huo umeweza kuunganisha vikundi na kuvipatia fursa za kiuchumi na kijamii kwa kutoa mafunzo na semina mbalimbali za wanavikundi ikiwa ni pamoja na mafunzo ya usindikaji, kuwaunganisha na huduma ya bima ya afya na ushiriki wa maonyesho ya biashara kwa ajili ya kutangaza bidhaa zao.

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment


Top