Mkuu
wa wilaya ya Manyoni, Fatuma Toufiq (wa kwanza kushoto) na anayefuata
ni Dc wa wilaya ya Iramba,Yahaya Nawanda na mkuu wa wilaya mpya ya
Ikungi, Manju Masambya (wa tatu kushoto)
Na Nathaniel Limu, Manyoni
SERIKALI
wilaya ya Manyoni mkoani Singida imeiomba serikali kuu kuangalia
uwezekano wa kurejesha mapema zoezi la oparesheni ‘tokomeza ujangili’,
ili kudhibiti kasi kubwa iliyopo ya majangili kuua wanyama pori hasa
tembo.
Ombi
hilo limetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni,Fatuma
Toufiq wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya wimbi kubwa la
majangili kuua wanyama pori na zaidi tembo katika hifadhi za wilaya
hiyo.
Amesema
kuwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita,majangili katika hifadhi
ya Rungwa,Kizigo na Kihesi wilayani humo yameuawa tembo 35.
Aidha,Mkuu
huyo wa wilaya amesema kuwa kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi wameweza
kukamata meno ya tembo mara mbili kati ya Januari na sasa katika
kizuizi cha kijiji cha Kayui kata ya Mgandu.
“Kama
hiyo haitoshi, hivi karibuni tena tumemkamata Afisa Mtendaji wa kijiji
cha Kayui Philemon Kanyonga na watu wengine wanne kwa tuhuma ya kumiliki
meno ya tembo kilo160 na bunduki ya kivita SMG moja pamoja na risasi
zake 195″, amesema.
Toufiq
amesema kutokana na kasi hiyo ya uwindaji haramu unaotishia ustawi wa
wanyamapori wakiwemo tembo,upo umuhimu mkubwa wa oparesheni tokomeza
ujangili ikarejeshwa mapema iwezekanavyo.
Naye
Juma Kidimanda mkazi wa Singida mjini,ameiomba serikali iache kujivunia
vitendo vya kutangaza tu kukamata nyara za serikali ikiwemo meno ya
tembo bali ijikite zaidi katika kuongeza juhudi za kudhibiti vitendo vya
uwindaji haramu wa wanyamapori.
“Hizi
adhabu wanazopewa majangili wanaotumia silaha za kivita kuulia
wanyamapori,nina wasi wasi nazo.Inaelekea sio kali kulingana na makosa
wanayoyafanya.Napendekeza serikali ianzishe adhabu kali zaidi
ikiwezekana ya kifo ili kuwaogofya majangili waweze kuachana na uwindaji
haramu na kutafuta njia nyingine ya kujiingizia mapato”,amesema Juma.
No comments: