Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MAKAMU
mwenyekiti wa zamani wa Yanga sc, Bilionea, Davis Mosha ameushutumu
uongozi wa sasa wa klabu hiyo kushindwa kuwabakiza wachezaji muhimu
kikosini kuelekea msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara na michuano
ya kimataifa.
Mosha
ambaye ni mwanachama na shabiki mkubwa wa Yanga, ameshangazwa na
uongozi wa klabu hiyo chini ya mwenyekiti Yusuf Manji kumwachia kiungo
wake mkabaji, Frank Domayo na mshambuliaji Didier Kavumbagu kwenda Azam
fc.
“Tunajua Kavumbagu kaenda kule, labda ndiye walikuwa wanamhitaji”.
“Haya, tumekuja kusikia Domayo naye kaenda Azam, mara tunasikia fununu kuwa Mbuyu Twite naye anakwenda Azam”.
“Sasa
ni nini kinaendelea hapa katikati, ni kwamba viongozi wanataka kuondoka
na kuacha timu haina wachezaji kwasababu wamesema hawagombei tena au
wanataka kuleta wachezaji wazuri zaidi kuliko hao”. Alisema Mosha kwa
masikitiko makubwa.
“Yanga
iliyoanzishwa mwaka 1934 haina uwanja. Timu ya Azam iliyoanzishwa juzi
ina uwanja, timu ya Azam ina TV, timu ya Azam imekuja juzi sasa
inachukua wachezaji Yanga. Hii ni aibu, sisi ndio tunatakiwa kuchukua
wachezaji Azam”.
“Itafika
mahali tutabaki tuna historia ya wanachama nchi nzima, lakini hatuna
maendeleo yoyote. Kama Azam wanachukua wachezaji wetu manake itafika
wakati na wanachama watahamia Azam”.
Akizungumzia
kuhusu kuwa kiongozi wa Yanga kwa mara nyingine, Mosha alisema hana
kinyongo kuwa kiongozi wa klabu hiyo kwasababu yeye sio kiongozi, lakini
bado wanamfuata na hilo ndilo jambo la msingi zaidi.
“Sio
unaonekana kiongozi halafu hauisaidii Yanga. Mimi nina mapenzi na
Yanga, sijawa na mapenzi na yanga jana au leo, nimekuwa na mapenzi na
Yanga miaka mingi”.
“Na
ndio maana wana Yanga wengi wananikubali, mambo ya Yanga mimi nabishana
mpaka mwisho, nabishana mpaka kufa kuhusu Yanga. Siwezi kusema labda
kwasababu nyie waandishi mnaniuliza”.
“Devis Moshi ni Yanga na nitaendelea kuisaidia Yanga. Si kwasababu ya kipato nilichonacho, hata kabla ya kipato”.
“ Kama unakumbuka historia ya nyuma, mimi nimekuwa nikiisapoti Yanga tangu nikiwa timu ya Ushirika ya Moshi”.
Aidha,
Mosha amewataka wanachama kuwa makini kuelekea uchaguzi ujao
utakaofanyika mwezi juni mwaka huu ili wasichague bora kiongozi
kwasababu wamejifunza.
Alisema
wasimchague mtu kwasababu labda sura yake ni nzuri na amejipaka mafuta
wakaona anafaa, bali waangalie watu wenye historia na mapenzi ya Yanga.
“Tumechukua watu wasiojulikana, hatimaye Yanga yetu inakufa”.
“Mimi nilitoka kwenye uongozi baada ya kuona nina watu wasioipenda Yanga, nikaona nisije kuchafua jina langu”.
“Ushauri
wangu ni kwamba kiongozi anayekuja Yanga awe ni Yanga na awe anaipenda
Yanga na awe anatoa muda wake mwingi kuisaidia Yanga”.
“Usitake
kuwa kiongozi kwa kutaka jina, awe kiongozi kwa kuonesha mapenzi yake
na nia yake ya kuisaidia timu. Asije akachukua uongozi halafu kesho
akaona unamkera na kuamua kufanya mambo yake”. Aliongeza Mosha.
No comments: