Dar es
Salaam. Jaribio la kuzipandisha klabu za Mwadui na African Lyon
kinyemela limegonga mwamba baada ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kugoma kuongeza timu za Ligi Kuu hadi
16 msimu ujao wa 2014/2015.
TFF
ilitaka kuongeza timu hadi kufikia 16 kwa lengo la kuipoza Mwadui ambayo
ilipokwa nafasi ya kucheza Ligi Kuu baada ya Stand United kupewa pointi
za mezani siku ya mwisho ya Ligi Daraja la Kwanza, wakati uongozi wa
African Lyon unahusishwa kuwa na uhusiano wa karibu na ‘bosi’ mmoja wa
TFF.
Habari
ambazo gazeti hili limezipata zinasema wajumbe hao walikataa mapendekezo
ya Kamati ya Mashindano ya TFF, ambayo ilitaka msimu ujao Ligi Kuu iwe
na timu 16, kwa kuziongeza timu hizo mbili zilizoshika nafasi za juu
kwenye makundi yao.
Kamati
hiyo pia ilikuwa ikiendesha kampeni ya kuhakikisha Ashanti United
inabakizwa Ligi Kuu pamoja na Rhino Rangers na JKT Oljoro.
Hata
hivyo, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF walikataa mapendekezo hayo
na badala yake wakapitisha msimu wa 2015/2016 ndio ligi iwe na timu 16
badala ya 14.
“Hatuwezi
kubadili kanuni baada ya msimu kumalizika, hivyo Ligi Kuu inayoanza
mwezi wa nane tumeamua itabaki na timu 14 kama kawaida. Lakini msimu wa
2015/206 itakuwa na timu 16,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya
Utendaji ya TFF.
“Pia
tumeipa jukumu Kamati ya Mashindano ya TFF iandae marekebisho kisha
watuletee na sisi tutapanga kanuni za ligi kwa ajili ya msimu ujao.
“Kuna
mapendekezo kuwa msimu ujao zishuke timu mbili kisha zipande nne, na
mapendekezo mengine ni kushusha timu tatu na zipande tano,” alisema
mjumbe huyo.
Taarifa
iliyotumwa na ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura inasema kuwa uamuzi
wa kuongeza timu msimu wa 2015/16 umefanywa kwa lengo la kuongeza
ushindani katika ligi hiyo na kuwawezesha wachezaji kupata mechi nyingi
zaidi.
“Kwa
mabadiliko hayo maana yake ni kuwa Ligi Kuu msimu wa 2015/16 utakuwa na
mechi 240, wakati kwa sasa una mechi 182,” alisema Wambura.
Katika
hatua nyingine, habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kamati hiyo
ya utendaji itapitisha adhabu kwa mtu au klabu itakayopatikana na hatia
ya kupanga matokeo.
“Kumekuwa
na upangaji wa matokeo sana katika ligi, msimu ujao atakayebainika
anaweza kufungiwa miaka 10 hadi 20 au maisha,” alisema mmoja wa wajumbe
wa Kamati ya Utendaji.
Wakati huohuo, Wambura alisema Kamati ya Utendaji itafanyia uamuzi mapendekezo ya idadi ya wachezaji wa kigeni.
katika
eneo hilo baada ya kupata maoni ya klabu za VPL na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL), ambazo Mei 11 mwaka huu zitakutana na Rais wa TFF, Jamal
Malinzi.
“Mapendekezo
ya Kamati ya Mashindano ni kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni iendelee
kuwa watano kama ilivyo katika kanuni za sasa za VPL,” aliongeza
Wambura. (CHANZO: MWANANCHI)
No comments: