Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amechaguliwa kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi katika Maendeleo
Barani Afrika kwa mwaka 2013 .
Heshima
hiyo kwa Rais Kikwete imetolewa na jarida maarufu la kimataifa la
African Leadership Magazine Group na Tuzo la heshima hiyo itatolewa
jioni ya kesho, Jumatano, Aprili 9, 2014, katika sherehe iliyopangwa
kufanyika Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C ikiwa ni pamoja na
chakula cha jioni.
Tuzo hiyo
itapokelewa kwa niaba ya Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe, ambaye tayari
amewasili mjini Washington kwa sherehe hiyo kubwa.
Tuzo hiyo
ya heshima kubwa hutolewa kwa viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango
mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao na
limetolewa kwa Rais Kikwete kwa mwelekeo wake usiokuwa wa kawaida na
wenye mafanikio makubwa kwa masuala ya utawala bora.
Jarida hilo
linasema kuwa ukweli wa hali hiyo bora ya utawala bora chini ya
uongozi wa Rais Kikwete umeendelea kumiminiwa sifa kimataifa na leo
umeifanya Tanzania kuwa nchi ya kuigwa mfano kama kituo cha uhakika cha
uwezeshaji kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa katika sera na
mifumo ya uchumi.
Jarida hilo linasema kuwa Rais Kikwete alikuwa chaguo kubwa na la kwanza
la wasomaji wa Jarida hilo ambao walipiga kura kupitia njia mbali mbali
za mawasiliano za jarida hilo.
Linasema Jarida hilo, “Kuhusu
maoni ya wasomaji wetu juu ya kiongozi yupi wa Afrika ambaye ni hodari
zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na maendeleo, matokeo ya majibu ya swali
hilo yamedhihirisha bila shaka yoyote kuhusu nafasi ya Rais Kikwete
katika uongozi wa nchi yake. Na ushahidi uko kila mahali – ameweza
kusimamia uchumi ambao umekuwa kwa wastani wa asili mia saba kwa miaka
yote ya uongozi wake.”
Sherehe za
kesho, miongoni mwa mambo mengine, zitaliwezesha Jarida hilo kutangaza
mafanikio ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete kwa Jumuia ya
Kimataifa, ikiwa ni pamoja na Jumuia ya Kimataifa ya Kibiashara,
wanadiplomasia na taasisi nyingine zenye ushawishi mkubwa katika medani
za kimataifa na zenye makao yake katika Jiji la Washington na maeneo ya
jirani
No comments: